BABU.
Mwanangu keti kitako, ‘sikiye wangu wosia,
Kwani sikosi ukoko, nitakayo kuambia,
Maishayo sokomoko, nyongo utatumbukia,
Na utapigwa kiboko, na maisha uje lia,
Mwenendo wako mwanangu, umeingia dosari,
MJUKUU.
Kigoda nimekalia, tayari kukusikia,
Ni wapi nimekosea, cheche unanitupia?
Kila siku ‘mezoea, naona wanichukia,
Umesikia umbea, nao ukakuingia!
Uyaweke paruwanja, tujue mbivu na mbichi,
BABU.
Kimekujaa kiburi, ndaro pamoja mikogo,
Hilo silo jambo nzuri, hapo ulipo mdogo,
Kila nikikushauri, waliona jambo dogo,
Wadharau wangu umri, waniona mi’ mdogo,
Usiyapuuze mwana, siku yaja ‘tajutia,
MJUKUU.
Ya watu wayasikia, bila na kuulizia,
Bongoni zakuingia, kauli zao za doa,
Chuki wamenijazia, mabaya kunitakia,
Kizimbani naingia, hukumu kuipokea,
Sasa Jaji endelea, mashtaka kunisomea,
BABU.
Uambayo yanakera, naona umewehuka,
Waongozwa na hasira, wanionyesha kumaka,
Mwana aso na busara, mwisho wake kuanguka,
Hasira huwa hasara, na hili vyema kumbuka,
Punguza hizo papara, ubwabwa hujakutoka,
MJUKUU.
Vileo ninatumia, kitambo nilizamia,
Ni lipi utanambia, mimi navyo furahia?
Shuleni nilikimbia, uhuru kujipatia,
Niliko nafurahia, amani imenijia,
Mawazoni mwajitia, ya kwangu kufwatilia,
BABU.
Ninakuonya sikia, ‘situmbukie dimbwini,
Mengi nimeyapitia, papa hapa duniani,
Ili usije jutia, tia haya maanani,
La sivyo kitaingia, kitumbua mchangani,
Mema ninakutakia, akujalie Manani,
MJUKUU.
Ni mengi nimeyafanya, ninakubali hakika,
Aghalabu ‘menionya, najutia kuwehuka,
Vya kutosha ‘menikanya, na sasa nimekanyika,
Nilikuwa kama panya, kutawala ‘lipondoka,
Toka leo nabadili, mwenendo wangu daima,
MTUNZI: Malenga Mtanashati
ENEO: Kesogon
©️2025✍️