Alipoondoka baba, mama kuachwa mjane
Ya baba yote akiba, walisema wagawane
Hatukupewa na haba, tuliachwa na ujane
Tulisalia kulia, kilio kisicho dawa
Mama akawalilia, huruma akaonewa
Mahali pa kulimia, shamba dogo kukapewa
Tulikuwa tu wadogo, yote yakifanyika
Mama na ndugu mdogo, kwenye shamba tukafika
Kulailima mihogo, mahindi na kadhalika
Walikujia mazao, siku yetu tukivuna
Wakaipeleka kwao, tukawa chetu hatuna
Yamo kwenye shamba lao,mashangazi wakanena
Hima hatukufa moyo , tuliyaishi maishi
Nayo tulokuwa nayo, matumbo ikashibisha
Mama kitutia moyo, yote hayo yangeisha
Mkopo alichukua, mama tukaenda shule
Asingelipa hatua, shamba letu lijendele
Nasi ikawa satua, shuleni twende kilele
Tulisoma tukilima, huku tukivumilia
Kwa walimu taadhima, sisi tukachikilia
Ilipofika hatima, mosi tukaimbukia
Tulipata wafadhiri, tukaenda sekondari
Tukakizika kiburi, masomo tukakariri
Huko tukapata heri, gredi nzuri fahari
Chuoni tulipofuka, kina ami walikuja
Kutuchukua hakika, tuliokuwa pamoja
Tukakatakaa fika, na vyao vingi vioja
Tuliosoma yakini, ndugu akawa daktari
Mimi nami runingani, nikawa mwanahabari
Mama akawa usoni, tabasamu lashamiri
Wote waliotuona, midomo walifungua
Walosema tuna la’na, walishindwa kutambua
Wakawa wasemezana, huku wakitwangalia
Na sisi tumejifunza, kwa amani tukaishi
Na mama alotutunza, apate nzuri aushi
Daima ni Mungu kwanza, kisha mametu shabashi
Wanjohi. P. Mugambi
Malenga Kitunguu Machoni